Call: +255 22 2668992

BARAZA OUT, LARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA CHUO.

baraza-out-laridhishwa-na-utendaji-kazi-wa-chuo

Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), limeridhika na utendaji kazi wa vitengo mbalimbali vya chuo ambao unachagizwa na ubunifu, ushirikiano, weledi, maarifa, ujuzi, uzingativu wa maadili, sheria, kanuni na miongozo na nidhamu ya hali ya juu ya watumishi wake.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya wajumbe wa Baraza la OUT waliohudhuria kikao cha 119 cha baraza hilo uliofanyika Aprili 5, 2024 na kisha kutembelea vitengo mbalimbali vilivyopo Makao Makuu ya Chuo, Kinondoni jijini Dar es Salaam kujionea kazi mbalimbambaili za chuo zinavyoendeshwa.

Akizungumzia ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Prof. Sylivia Temu ameipongeza Menejimenti ya OUT kwa kusimamia vyema utendaji wa chuo na kuleta matokeo chanya yenye tija kwa taifa na kimataifa.

 “Wajumbe wa Baraza tumepata fursa ya kutembelea vitengo vya Huduma za Maktaba, Kurungezi ya huduma za mafunzo na mitihani, Kurugenzi ya Udahili wa Taaluma za awali, kurugenzi ya shahada za Umahiri na Uzamivu, kitengo cha teknolonia saidizi kwa watu wenye mahitaji maalumu na kituo cha mkoa wa kichuo Kinondoni. Tumejifunza mambo mengi sana kuhusu utedaji kazi katika vitengo hivyo. Tumeridhika na mambo yanayofanywa na chuo katika kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na yenye viwango vya juu kukidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa.” amesema Prof. Temu.

Aidha, amesema Wajumbe wa Baraza wamevutiwa na huduma za mafunzo zinazotolewa na kitengo cha teknolojia saidizi kinachowafundisha watu wenye changamoto ya uoni na wasiosikia kutumia mifumo ya teknolojia ya habari na mawasilianao (TEHAMA) katika kuwasiliana. Jambo lililowafanya wajumbe hao kuomba taarifa zaidi ili nao wasaidie kupatikana kwa wahisani watakaokuwa tayari kufadhili mafunzo hayo na kuhakikisha yanaendelea kutolewa bure kwa wote.

Baraza hilo limetembelea majengo ya OUT katika kituo cha mkoa wa kichuo cha Kinondoni ambayo yamenunuliwa na serikali na kuwa mali ya Chuo kuona namna ya kutumia eneo hilo kwa mawanda mapana zaidi ili kuwezesha chuo kupitia kituo hicho cha Kinondoni kutoa huduma kwa wanafunzi wengi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amelishukuru Baraza la Chuo kwa kuamua kufanya ziara ya kutembelea vitengo vya Chuo ili kujionea utendaji kazi na kutoa maoni ya namna ya kuimarisha zaidi huduma za Chuo kwa wanachuo wake. 

Amesema, “Baraza ndicho chombo cha juu kabisa katika uendeshaji wa chuo, kufanyika kwa ziara hii ni sehemu ya Baraza katika kukisimamia Chuo na kukipatia miongozo maridhawa ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake. Umuhimu wa ziara hii ni kwamba wajumbe nao wamepata fursa ya kuendelea kukifahamu chuo pamoja na mahitaji yake katika miundombinu, kuongezwa rasilimali watu, mahitaji ya mtandao, vitendea kazi na kutoa njia ya upatikanaji wa mahitaji hayo,” amesema Prof. Bisanda.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri wa kitaalamu Prof. Deus Ngaruko, amelihakikishia Baraza, kwamba OUT ni kitovu cha ubunifu ambapo mihadhara ya Chuo inafanyika Mubashara kupitia mtandao wa ZOOM, matini za kufundishia na kujifunzia zimepakiwa kwenye mfumo wa MOODLE, wanafunzi wanajisomea na kujadiliana kupitia Vimbwette vya What’s App, Telegram, ZOOM, Google teams, mafunzo kwa vitengo, mitihani na kuhitimu kwa On Demand na Maktaba mtandao ya OUT kutaja kwa uchache.

Prof. Ngaruko, amedokeza kuwa mifumo hii ni zao la ubunifu wa watumishi wa OUT ambapo leo wanafunzi wanapata huduma za viwango vya hali ya juu wakiwa huko huko walipo wakiendelea na shughuli zao. Ni vyema kwa Baraza kujionea huduma hizi na kuendelea kuzifahamu zaidi kwani ni chachu ya kuongeza ubunifu wa OUT.

Katibu wa Baraza la OUT, Wakili Nelly Moshi, ametoa shukurani za dhati kwa wajumbe wa Baraza hilo kutenga muda wa kutembelea vituo vya Chuo ili kuona utendaji kazi wake. Kupitia ziara hiyo, wajumbe watakuwa na picha kamili ya OUT na kuisaidia Menejimenti katika kuimarisha na kutekeleza kikamilifu mpango mkakati wa chuo ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa OUT nchini Tanzania. 

Baraza limekutana katika kikao chake cha 119 chini ya Mwenyekiti wake Prof. Joseph Kuzilwa katika kikao chake cha kawaida na kisha kutembelea vitengo vya Chuo ili kujionea utendaji kazi. Hii ni ishara kwamba, Baraza la OUT linashirikiana na Menejimenti bega kwa bega katika kukiletea Chuo maendeleo endelevu.