Call: +255 22 2668992

KAMATI YA USHAURI WA KITASNIA OUT, YA FUNDWA

kamati-ya-ushauri-wa-kitasnia-out-ya-fundwa

Kamati ya Ushauri wa Kitasnia (IAC) ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, imejengewa uwezo katika utekelezaji wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET), katika mafunzo yaliyoandaliwa na Kamati ya Ushauri wa Kitasnia ya kitaifa yaliyofanyika katika kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kuanzia 

 hadi , 2023.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, mgeni rasmi na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Kennedy Hosea, amezitaka kamati hizo zitoe ushauri ambao utaleta mabadiliko ya kweli ili nchi iweze kufikia lengo la kuwa na wahitimu wa elimu ya juu wenye weledi wa kutosha kukabiliana na hali ya mabadiliko ya ajira nchini.

“Kamati zote mtoe ushauri ambao utaleta mabadiliko tunayoyataraji, mkifanya hivyo mtalisaidia Taifa kusonga mbele. Pia, mitaala mipya iakisi elimu ujuzi, mazingira na mahitaji ya jamii ili ichangie kutoa suluhisho za changamoto zinazozikabili jamii katika maeneo ambako kampasi mpya zinazojengwa” Amesisitiza Dkt. Hoseah.

Aidha, Mratibu Msaidizi wa mradi wa HEET, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Timothy Lyanga, amesema mafunzo haya yamekuwa ni muhimu sana kwa kamati za Kitasnia katika kutekeleza majukumu yao. Mawasilisho yaliyotolewa yamewapatia miongozo mbalimbali ambayo wataitumia katika kuongeza weledi wakati huu wa mabadiliko ya mitaala.

“Mabadiliko ya mitaala yanaendelea vyema, idara mbalimbali zinafanya hiyo kazi na wapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Hivyo, mawasilisho yametujenga katika kuimarisha mitaala ya chuo hiki ambapo tunazingatia weledi mkubwa ili kutoa wahitimu bora wa elimu ujuzi wenye kuweza kuanzisha miradi, kuajirika na wenye uwezo wa kuishauri jamii na serikali kwa ujumla.” Amesema Dkt. Lyanga.

Kamati za ushauri wa kitasnia, zimeanzishwa ili kushiriki moja kwa moja katika mabadiliko ya mitaala ya Elimu ya juu nchini kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia. Vyuo vikuu, taasisi za kielimu na mamlaka za elimu kwa pamoja zinafanya mabadiliko makubwa ya mitaala ya elimu ya juu ili kuwa na mitaala yenye kuzalisha wahitimu bora wenye weledi wa kukidhi matakwa ya soko la ajira.