Call: +255 22 2668992

OUT KUBORESHA MIFUMO YA TEHAMA KUIMARISHA UFUNDISHAJI.

out-kuboresha-mifumo-ya-tehama-kuimarisha-ufundishaji

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimedhamiria kuboresha mifumo ya TEHAMA ya kufundishia kwa kuingia mkataba wa makubaliano na Chuo Kikuu Huria cha Uswisi unaolenga kuimarisha ushirikiano katika maswala ya tafiti na maendeleo kwenye eneo la ujifunzaji na ufundishaji unaotumia teknolojia ya kisasa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo iliyofanyika Aprili 24, 2024 makao makuu ya chuo Kinondoni jijini Dar Es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Prof. Elifas Tozo Bisanda amesema ushirikiano huu unaendana na mahitaji ya nchi kwa sasa kwani utaenda kuboresha huduma za TEHAMA katika utoaji wa elimu huku ukilenga kukidhi uhitaji wa kuhudumia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

“Tunataka kwenda hatua ya mbele zaidi ya kumwezesha mwanafunzi kufanya mtihani moja kwa moja kupitia TEHAMA na utasahihishwa kupitia TEHAMA pia, kwa hatua hizi tunategemea kuachana na walimu kwani TEHAMA itafanya kila kitu. Kwa maana hiyo hata ukiwa na wanafunzi wengi hautachelewa kusahihisha hii itarahisisha na kuongeza nguvu kazi itakayoendana na uhitaji wa chuo ambapo itatoa nafasi ya kuweza kudahili wanafunzi wengi na kuwahudumia wote kwa pamoja.” Amesema Pof. Bisanda.

Akiongea katika hafla hiyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Uswisi, Prof. Egon Werlen, amesema kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani kumekuwa na wimbi la matumizi ya simu janja. Katika nchi zilizoendelea wanafunzi hujikita zaidi kutoa na kupokea taarifa kwa kutumia teknolojia ya simu japo teknolojia hiyo hiyo imekuwa ngumu katika utoaji elimu.

“Ongezeko la mabadiliko na maendeleo ya Teknolojia yanatufanya nasi tubadilike tuendane na mahitaji ya sasa ya dunia, wanafunzi wanaona bora kukaa nyumbani na kusoma kupitia mtandao na hata mitihani kufanya kupitia mtandao. Kutokana na mabadiliko haya kunakuwa na umuhimu wa kuboresha huduma za TEHAMA ili kuendana na kasi ya teknolojia,” amesema Prof. Werlen.

Naye Dkt Evaristo Mtitu akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, amepongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kuingia katika mkataba wa makubaliano na chuo cha Kikuu Huria cha Uswisi katika kuendelea kuwekeza kwenye matumizi ya TEHAMA kama wizara inavyohimiza. Hili ni jambo zuri linakwenda kutatua changamoto ya uhaba wa wanataaluma iwapo litatumika vyema na litatoa fursa kwa mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja na wanafunzi kushiriki kikamilifu katika kujifunza.

Ameendelea kusisitiza kuwa ni muhimu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kikawa na mkakati endelevu kuhakikisha ushirikiano huu unatekelezeka, haya makubaliano yasiishie kwenye mahusiano ya vyuo vya ndani na nje tu. Yaende kwenye vyuo vingine vya ndani tuone maeneo mahususi ya ushirikiano kwenye vyuo vyetu kwanza ndipo tutanue mawanda ya ushirikiano na ya teknolojia kwenye majukumu mengine ya kichuo kama ufundishaji na ujifunzaji, utafiti na utoaji wa huduma kwa jamii.

Hafla hii imefanyika makao makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilichopo Kinondoni jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka pande zote mbili za vyuo vya OUT na Uswisi.