Call: +255 22 2668992

PROF. BISANDA: OUT KUJENGA MAKAO MAKUU DODOMA.

prof-bisanda-out-kujenga-makao-makuu-dodoma

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kinatarajia kujenga Makao Makuu yake katika Makao Makuu ya nchi Dodoma katika eneo la ekari 60 Msalato jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa OUT Prof. Elifas Tozo Bisanda katika ziara ya wajumbe wa Baraza la Chuo walipotembelea eneo hilo leo tarehe .

Prof. Bisanda amesema “kutolewa kwa eneo hilo la ujenzi wa Makao Makuu ya OUT ni kufuatia maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango aliyoyatoa kwa Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kutoa ardhi ya kutosha kwa OUT kujenga Makao Makuu yake. Hatua za mwisho za OUT kumilikishwa eneo hili zinaendelea na baada ya hapo ujenzi utaanza kwa fedha kutoka serikalini, wadau wa elimu na OUT kufanya jitihada za kujiongeza.”

Aidha, Prof. Bisanda ameishukuru ofisi ya Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kwa kutekeleza ahadi na maelekezo ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango aliyoyatoa tarehe katika ziara yake aliyoifanya OUT.

Nao wajumbe wa Baraza kwa umoja wao, wamefurahia sana kufika na kuliona eneo hilo na kuuelekeza uongozi wa chuo kuhakikisha hatua za umilikishwaji zinakamilika mapema iwezekanavyo. Vile vile wajumbe wameishukuru serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia OUT eneo la kujenga Makao Makuu yake Dodoma na kwamba hili ni jambo kubwa sana kwa maendeleo ya nchi yetu.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Baraza Prof. Suleiman Ngware amesema, “Tunaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia eneo hili la ujenzi wa Makao Makuu ya Chuo chetu hapa Dodoma. Ni heshima kwa OUT kuwa na Makao Makuu Dodoma kwa sababu hiki ndicho Chuo ambacho kina vituo nchi nzima na hapa Dodoma ndipo Makao Makuu ya Nchi. Pia, OUT ni Chuo cha kimkakati ambapo kuanzishwa kwake ni kwa ajili ya kuwafikia watu wengi kule walipo wakiwa kazini na katika biashara na shughuli zao, kikiwa na Makao Makuu Dodoma kinajenga taswira hiyo kwa ukamilifu wake.”

Wajumbe wa Baraza la Chuo wapo jijini Dodoma kwa ajili ya kikao cha Baraza cha 116 kitakachofanyika tarehe 23/06/2023 katika chuo cha OUT Dodoma.