Call: +255 22 2668992

TAARIFA ZA WAHITIMU NI MUHIMU KUZALISHA MITAALA BORA.

taarifa-za-wahitimu-ni-muhimu-kuzalisha-mitaala-bora

Makamu Mkuu wa chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutoa taarifa zinazohitajika ili ziweze kusaidia katika kuandaa mitaala iliyo bora zaidi itakayosaidia kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa umahiri na kuzalisha ajira. 

Prof. Bisanda, amesema hayo Juni 13, 2023 makao makuu ya chuo hiki Kinondoni jijini Dar es Salaam, alipoitisha mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia hilo.

“Tunahitaji mitaala inayokuja ilenge mahitaji halisi ya jamii kulingana na maendeleo makubwa ya teknolojia yanayobadilika kwa kasi hivi sasa, kinachofanyika ni kutathmini upya mitaala iliyopo ili kubaini kama elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya mabadiliko ya sasa ili yasaidie kutengeneza mitaala yenye kuzalisha wahitimu wenye kukidhi mahitaji ya jamii.” Amesema Prof. Bisanda.

Aidha, alisisitiza kuwa njia za kimtandao zinazotumika kukusanya taarifa hizo zimekuwa zikisambazwa katika mitandao, tovuti na mitandao ya kijamii ya chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambapo waajiri na wahitimu watumie fursa hiyo kutoa taarifa sahihi kwa mustakabali wa ubora wa elimu inayotolewa na chuo hiki lakini pia elimu ya Tanzania kwa ujumla.

Ukusanyaji wa Taarifa za Wahitimu na Waajiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania unaratibiwa na chuo hiki chini ya udhamini wa mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi nchini kupitia Elimu ya juu unaodhaminiwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuendana na sera ya serikali inayotaka kuzalisha watahiniwa wenye uwezo wa kujiajiri na kuzalisha ajira.