Call: +255 22 2668992

WAJUMBE WA BARAZA LA CHUO KIKUU HURIA WAAGWA DODOMA

wajumbe-wa-baraza-la-chuo-kikuu-huria-waagwa-dodoma

Wajumbe wa Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, wanaomaliza muda wao katika kulitumikia baraza hilo wameagwa katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa chuo hiki kituo cha mkoa wa Dodoma.

Hafla hiyo, ilihudhuriwa na Mkuu wa chuo, Mhe. Mizengo Pinda, pamoja na menejimenti ya chuo imefanyika Juni 22, katika jiji la Dodoma ikiwa  ni sehemu ya wajumbe wa baraza  hilo kufanya shughuli nje ya makao makuu jijini Dar es Salaama ili kujionea namna vituo vya mikoa vinavyotekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi katika kufundisha, kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Pinda, amesema wajumbe wanaomaliza muda wao wana kila sababu ya kupongezwa kwa kuwa wamekuwa wakijitoa kwa muda, nguvu na maarifa yao yote ili kuhakikisha chuo kinakuwa mahali pazuri katika kutekeleza mpango mkakati wake kwa mafanikio makubwa.

“Ninachojivunia kwa chuo hiki ni kuona jitihada za kuendeleza hivi vituo kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi huko huko waliko badala ya wao kufuata chuo, jamii sasa inakielewa vyema chuo hiki na hii ni ishara kuwa timu hii imefanya kazi nzuri na kubwa. Tuendelee kuchapa kazi kwa uadilifu na timu itayokuja iendeleze haya haya mazuri na kubuni mengine mazuri zaidi kwa chuo chetu.” Alisema Mhe. Pinda.

Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Joseph Kuzilwa, akilipongeza baraza hilo linalomaliza muda wake, amesema taarifa mbalimbali za chuo zimeonyesha uwepo wa mafanikio makubwa ambayo kwa hakika baraza hilo limekuwa ni chachu ya mafanikio hayo kwa kipindi chote cha uhai wake.

“Licha ya changamoto kadha wa kadha lakini mpango mkakati wa chuo unaoisha muda wake katika mwaka fedha 2022/23 umeweza kutekelezwa kwa zaidi ya asilimia sabini, na hayo yote ni matokeo ya usimamizi mzuri wa baraza hili ambalo jukumu lake kubwa ni kusimamia utekelezaji wa mpango mkakati wa chuo ili kiweze kufikia malengo ya kuanzishwa kwa chuo ya kuwahudumia wananchi huko huko walipo bila kuacha kazi, biashara na shughuli zao za ujenzi taifa na jamii kwa jumla tena kwa gharama nafuu. ” Amesema Prof. Kuzilwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema tofauti ya Chuo hiki na vyuo vingine ni kwamba Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinamfuata mwanafunzi badala ya mwanafunzi kufuata chuo, hivyo tumedhamiria huduma zetu ziende chini hadi kufikia ngazi ya kata na hata ikibidi tufike katika ngazi ya kijiji.

“Katika mwaka wa fedha 2023/24, tumefanikiwa kutengewa fedha za maendeleo kutoka serikalini kiasi cha shilingi bilioni moja ambacho tutakitumia katika kuimarisha vituo mbalimbali vya mikoa tulivyonavyo. Pia, tuna dhamira ya kujenga jengo  la kituo cha Pemba ambako tayari tuna eneo letu na idadi ya kutosha ya wanafunzi.” Alimaliza kusema Prof. Bisanda.

Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania limefanya mkutano wake wa 116 jijini Dodoma tarehe 23 Juni, 2023 ambapo katika mkutano huu baadhi ya wajumbe ndiyo mkutano wao wa mwisho baada ya kutimiza vipindi viwili vya ujumbe.