Call: +255 22 2668992

WATAALAM WA USTAWI WA JAMII MASHULENI, MWAROBAINI WA MATATIZO YA UKATILI KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM.

wataalam-wa-ustawi-wa-jamii-mashuleni-mwarobaini-wa-matatizo-ya-ukatili-kwa-watoto-wenye-mahitaji-maalum

Katika kukabiliana na matatizo ya ukatili yanayowakabili watoto wenye mahitaji maalum mashuleni, serikali imeshauriwa kuajiri wataalamu wa Ustawi wa Jamii katika shule za msingi nchini ili kutatua matatizo mbalimbali wanayopitia watoto hao mashuleni na katika jamii zinazowazunguka.

Wito huu umetolewa na Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dkt. Mariana Makuu, walipokutana kufanya tathmini ya mradi wa kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya vyuo viwili vya nchini  Norway, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Ualimu, Elimu Maalumu – Patandi cha mkoani Arusha Machi 27, 2024 Makao Makuu ya Chuo hiki yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kilichowakutanisha washiriki kutoka nchini Norway, wahadhiri, maofisa maendeleo ya jamii na wadau mbalimbali wa maswala ya ustawi wa jamii.

 “Mtoto mwenye mahitaji maalum awapo shuleni anatakiwa kulelewa kwa kupata huduma tatu muhimu ikiwemo elimu, afya na msaada wa kisaikolojia na kijamii (psycho-social support). Kundi la watoto wenye uhitaji maalum linakabiliwa na ukatili wa aina mbalimbali unaopelekea watoto hawa kukabiliwa na matatizo ya kisaikolojia. Uwepo wa Wataaam wa Ustawi wa jamii mashuleni wenye jukumu la kuangalia maswala ya kijamii kwa watoto hawa wakisaidiana na walimu wataweza kuibua na kuzuia ukatili na matatizo mengine yanayowakabili watoto hasa wale wenye ulemavu. Serikali ione umuhimu wa kuwaajiri wataalam hawa ili kuendana na mabadiliko ya jamii kwa sasa,” amesema Dkt. Makuu.

Aidha, akizungumzia ziara waliyoifanya nchini Norway hivi kribuni, Dkt. Makuu amesema shule za wenzetu zimefanikiwa kuwa ni sehemu salama kwa watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwa zina uwepo wa huduma za ustawi wa jamii jambo linalosaidia kugundua viashiria vya vitendo vya ukatili kwa watoto hao na kuvidhibiti mapema. Pia wataalam wa Ustawi wa jamii wamefanya jukumu la malezi kuwa jepesi kwa kushirikiana kwa ukaribu na walimu wa mtoto na wazazi.

Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Kinondoni, Silider Ussuma ameongeza kuwa endapo serikali itaongeza uwepo wa wataalam wa Ustawi wa jamii mashuleni wakiungana na walimu kwa pamoja watasaidia kuimarisha malezi ya watoto na hivyo kupunguza uwepo wa sonona miongoni mwao.

Akizungumza kwenye kikao hicho amesema “Watoto wenye mahitaji maalum wanahitaji upendo na kusikilizwa, changamoto zinazowaathiri hawa watoto miongoni mwao ni migogoro ya kifamilia. Bado nauona uhitaji mkubwa wa wataalam wa Ustawi wa jamii mashuleni ili kuondoa athari hizi kwa watoto hawa na kuwajengea uthubutu waweze kupenda shule na kufanya vyema”.

Mtalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Stella Shayo, ameshauri uwepo wa daftari maalum la kuwatambua na kuwasajili watoto wenye mahitaji maalum kuanzia ngazi ya mtaa, kata na hata wilaya ili serikali kupitia wataalam wa ustawi wa jamii iweze kufanya ufuatiliaji katika kaya kuhakikisha watoto hawa wanapata mahitaji yote muhimu na hawapati changamoto za ukatili wa aina yoyote ile.

Kikao hiki cha tathmini kimeratibiwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, kikilenga kufanya tathmini zenye kuleta utatuzi wa changamoto za watoto wenye mahitaji maalum mashuleni ili kuboresha huduma kwa kundi hilo wawapo mashuleni. Pia kuleta upatikanaji wa elimu bora katika mazingira bora kupitia mradi huu ambao una lengo la kusaidia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya haki ya mtoto na haki ya watu wenye ulemavu; mkazo ikiwa ni kuimarisha maisha ya watoto wenye ulemavu.